Abstract:
Lugha ni kipengele muhimu ambacho huwezesha kuwepo kwa mawasiliano miongoni
mwa watu. Katika juhudi za kurahisisha uwasilishaji na upokeaji wa ujumbe, ni muhimu
kuhakikisha kuwa lugha sahihi imetumiwa. Katika karne hii ya 21 ya mawasiliano ya sayansi na
teknolojia, suala la mawasiliano limeshika kasi kubwa kwa kila mtu. Kwa namna hii
mawasiliano yamekuwa ni jambo muhimu sana ambalo humwezesha mtu kupashana habari, taifa
kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi kuhusu matukio, na hata malengo na mikakati
iliyojiwekea. Iwapo makosa yatatokea katika maandishi au mazungumzo, mawasiliano kama
shughuli kuu ya kibinadamu hayatafaulu. Madhumuni ya makala haya ni kuchanganua makosa
ya kisemantiki yanayojitokeza katika mawasiliano andishi ya Kiswahili ya wanafunzi wa shule
za upili. Makala haya yametumia nadharia ya Uchanganuzi Makosa (Corder, 1967) kuonyesha
kuwa wanafunzi wanaojifunza lugha ya pili hufanya makosa ambayo yanaweza kubainishwa,
kuchanganuliwa, kuainishwa na kutathminiwa ili kubainisha mfumo unaofanya kazi. Data ya
makala haya ilikusanywa kutoka kwa wanafunzi wa shule za upili hususani kidato cha tatu,
kaunti ya Kakamega, nchini Kenya. Mbinu iliyotumiwa katika ukusanyaji wa data ni ya nyanjani
(hojaji na mjarabu). Katika kubainisha makosa husika, makala haya yametumia vielelezo
mbalimbali kutoka kwa watafitiwa lengwa. Makala haya pia yanatoa mapendekezo ya utatuzi wa
makosa yanayojitokeza katika matini za wanafunzi wa shule za upili. Makala haya yatawafaidi
walimu wa Kiswahili, wanafunzi wa shule za upili na vyuo vya elimu ya juu katika kurekebisha
makosa ya kisemantiki katika matini anuwai.