Abstract:
Lugha ya Kiswahili ina mfumo wa kifonolojia ambao una upekee unapolinganishwa na lugha
nyinginezo. Ingawa hii ni lugha ya Kibantu, kunadhihirika tofauti anuwai tunapolinganisha muundo wa
lugha hii na lugha nyingine za Kibantu katika kiwango cha kifonolojia. Tofauti hizi ndizo
zinazosababisha athari za kifonolojia ambazo zinadhihirika katika matumizi ya Kiswahili na wazawa wa
jamii mbalimbali za Kibantu. Makala hii inalenga kuweka wazi namna athari za kifonolojia
zinavyodhihirika katika mawasiliano andishi ya Wabantu wanapoandika maneno mbalimbali ya
Kiswahili. Aidha, njia sahihi ya kuyaandika maneno husika itasisitizwa. Data ya makala hii itatokana na
uchanganuzi wa mawasiliano andishi ya wanafunzi wa shule za Upili katika shule teule nchini Kenya.
Utafiti huu ulifanywa katika wilaya ya Nakuru na ulihusisha wanafunzi 100 wa kidato cha tatu kutoka
shule kumi teule. Mawasiliano husika yanahusu uandishi wa insha. Uchanganuzi unaoongeza data ya
makala hii ulifanywa kwa kuzingatia Nadharia ya Uchanganuzi Makosa (Corder, 1967). Matokeo ya
uchunguzi huu yatawasaidia wanafunzi wa taaluma ya Kiswahili, kwani makosa yatakayochanganuliwa
yatawawezesha kutofautisha kati ya Kiswahili sanifu na athari ya lugha mama katika Kiswahili. Kwa
walimu wa Kiswahili, mifano ya makosa itakayochanganuliwa itakuwa hazina mahususi ya
kuwawezesha kuwaelekeza wanafunzi wao kuhusu haja ya kuepuka makosa ya aina hiyo katika
mawasiliano andishi. Uchanganuzi husika pia utasaidia katika kuimarisha uchunguzi kuhusu matumizi
ya lugha ya Kiswahili, hususani kipengele cha uchanganuzi makosa.